Serikali imetoa jumla ya tani 372.4 za chakula kwa wilaya ya Bagamoyo ili kuweza kukabiliana na tatizo la Njaa
Na Anna Nkinda – Maelezo, Bagamoyo - 05/10/2009
Serikali imetoa jumla ya tani 372.4 za chakula kwa wilaya ya Bagamoyo ili kuweza kukabiliana na tatizo la njaa linaloikabili wilaya hiyo.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa wilaya hiyo Magessa Mulongo wakati akieleza hali ya chakula kwa mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika wilaya hiyo .
Mulongo alifafanua kuwa tani 186.2 ziligawiwa bure kwa wananchi na tani 186.2 zilitolewa kwa utaratibu wa kuuza ambapo kilo moja iliuzwa Tshs.50.
“Vijiji 64 kutoka katika kata 16 zenye jumla ya watu 132,703 wameombewa msaada wa chakula kupitia TASAF kwa mradi wake wa uhakika wa chakula (FOOD Security)”, alisema.
 |
Alizitaja sababu za wilaya hiyo kukabiliwa na njaa kuwa ni kutokana na mavuno hafifu msimu wa kilimo 2008/2009 kwani wilaya hiyo ina upungufu wa chakula cha mizizi na nafaka tani 39,270 na mikunde tani 6,356.
Aliendelea kusema kuwa thamani ya chakula ilifanywa na wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya tarehe 08 - 09/09/2009 ilibaini maeneo yaliyathirika kwa viwango vitatu tofauti.
Eneo lenye upungufu mkubwa wa chakula linajumuisha kata za Msata, Mbwewe, Kibindu, Miono, Mkange, Lugoba, Ubena, Chalinze na Tawalanda ambako kuna waathirika 112,144 na eneo lenye upungufu wa kati wa chakula linajumuisha kata za Vigwaza na Kiwangwa zenye waathirika 14,846.
Mkuu huyo wa wilaya aliendelea kutaja eneo lenye upungufu kidogo wa chakula ambalo linajumuisha kata za Dunda, Magomeni, Yombo, Kiromo na Zinga zenye waathirika 15,550 na kufanya jumla ya waathirika wote kuwa ni 142,540 sawa na asilimia 53 ya wakazi wote.
Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kutunza chakula walichonacho na kutokiharibu wakati wa sherehe za kuwacheza ngoma watoto wao
Mwenyekiti huyo wa WAMA aliendelea kuwasisitiza wakazi wa wilaya hiyo kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano huku wakitumia rasilimali zilizopo kama mito na ardhi yenye rutuba kulima chakula kwa wingi.
Siwakatazi kucheza ngoma, ngoma chezeni lakini muwe na matumizi mazuri ya chakula kwani mkiangalia hali halisi hivi sasa wilaya hii inkabiliwa na njaa hivyo basi kuna haja ya kutunza chakula kilichopo ”, alisema Mama Kikwete.
Alisema kuwa kama wataamua kutumia maji yaliyopo wanaweza kujipanga na kuzalisha chakula kingi ambacho kitawasaidia kuepukana na tatizo la njaa kama ilivyo hivi sasa.
Naye Mzee Athuman Khalifan ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Runga alisema kuwa wakazi wa wilaya hiyo wanakawaida ya kuwacheza ngoma watoto wao na kuwapa mafunzo ya aina mbalimbali ya jinsi ya kuishi na jamii hasa wakati wa kipindi cha mavuno na baada ya mafunzo hayo wanapika chakula la pombe kwa ajili ya kusherehekea
Huwa tunawacheza ngoma za aina mbalimbali kama bigirio, ngodo, mkole, mrao na bugi lakini kutokana na tatizo la njaa hivi sasa watu wengi hawawachezi ngoma watoto wao wanachofanya ni kuwapa mafunzo ya ndani pasipo kufanya sherehe yoyote ile na ukiona mtu anafanya sherehe basi ni yule mwenye uwezo kifedha”, alisema Mzee Khalifan.
Mama Kikwete anafanya ziara ya kikazi ya siku sita katika mkoa wa Pwani yenye lengo la kuchangia juhudi za kupunguza vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi kwa kutoa vifaa vya huduma ya afya ya uzazi, hususan katika wodi za wazazi. Kuhamasisha juhudi za maendeleo kwa wanawake kupitia vikundi vya SACCOS na benki za vijijini- VICOBA.
Kuhamasisha juhudi za kupunguza matukio ya mimba na utoro mashuleni, kuhamasisha vikundi vya Vyama vya Akiba na Kukopa (SACCOS) na benki za vijijini- VICOBA.
|