WAMA yaisaidia
vifaa vya hospitali Zahanati ya Kitunda, Wilaya ya Ilala Dar
es Salaam, Aprili 28, 2010
Na Philomena Marijani
Taasisi ya WAMA imetoa msaada
wa vifaa kwa hospitali ya Kitunda, iliyopo wilaya ya Ilala Mkoani
Dar es Salaam. Vifaa hivyo vilikabidhiwa na Mwenyekiti wa WAMA
Mhe. Mama Salma Kikwete kwa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kitunda
,Bi. Judith Philip. Vifaa vilivyokabidhiwa ni Vitanda vya hospitali
(Hospital Beds) 02, Magodoro (Mattresses) 02, Mashuka (Bedsheets)
04, Kifaa cha kupimia mwenendo wa upumuaji (Stethoscope) 01,
Kifaa cha kupimia shinikizo la damu (BP Machine) 01, Kifaa cha
kuwekea vifaa vya kujifungulia (Delivery Kit) 01, Mzani wa watoto
(Infant Scale) 01.
Katika hotuba yake katika Zahanati ya Kitunda Mama Salma aliomba
juhudi iongezwe katika uboreshaji wa afya ya uzazi kwa wasichana
na wakinamama pamoja na magonjwa ya Malaria na UKIMWI. Alisema
kuwa magonjwa haya bado ni changamoto katika nchi yetu.
WAMA imejiwekea utaratibu wa kutembelea Mikoa yote hapa nchini
ili kujionea maendeleo na changamoto ya mikoa hiyo na hatimaye
kutoa mchango katika maeneo makuu matatu: uboreshaji afya ya
uzazi ikiwemo kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na
uzazi, kuongeza ushawishi katika kuongeza fursa za Elimu kwa
watoto wa kike kwa kuzungumzia changamoto za matukio ya utoro
na ujauzito kwa Wanafunzi na kuwajengea uwezo Wanawake kiuchumi.
Katika ziara yake ya Wilaya ya Ilala WAMA pia ilitembelea Shule
ya Sekondari Jangwani, ambapo Mwenyekiti wa WAMA aliwasisitizia
wanafunzi wajitahidi katika masomo yao na wajiepushe na mitego,
vishawishi na matendo yanayoweza kuwasababishia matatizo.
“Msikubali vishawishi kwani peremende ya dk si sawa na asali
ya maisha. Iweje uridhie kuuharibu muundo/mpango wa maisha yako
kwa kitu cha mara moja ? Mnapaswa kuviepuka vishawishi na vitendo
vyote vinavyoweza kusababisha kuingia kwenye matatizo. Kumbukeni
haya ninayowaasa ili yawasaidie kuepuka vishawishi vya chipsi-kuku,
lifti, simu za mkononi mnavyorubuniwa navyo. Vishawishi vya
namna hii, havina lolote jema katika kukukomboa msichana kielimu,
kijamii na kiuchumi” Alisema Mama Salma
Mama Salma pia alipongeza uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam
kwa ongezeko la shule za sekondari za serikali na binafsi ambapo
katika shule za sekondari za serikali kuna ongezeko la asilimia
84% na shule za sekondari za binafsi kuna ongezeko la asilimia
53% kimkoa.
|