Wadau
wa maendeleo watakiwa kuwasaidia wanawake wajasiriamali, August
28,2011
Na Anna Nkinda – Maelezo
Wadau wa maendeleo hapa nchini wametakiwa kuwasaidia wanawake
wajasiriamali kwa kuwapa fursa zilizopo ndani ya uwezo wao kwani
wanawake hao huzalisha bidhaa za asili ya kitanzania ambazo hutumika
ndani na nje ya nchi na kwa kufanya hivyo huchangia kuongeza fursa
za ajira na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa juzi na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati
akizindua uchangishaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho
ya Tamasha la Wanawake Wajasiriamali Tanzania kwa mwaka 2011 lijulikanalo
kama Mwezi wa Wanawake Wajasiriamali (Month of Women Entrepreneurs
– MOWE) katika Hoteli ya New Afrika jijini Dar es Salaam.
Zaidi ya shilingi milioni 55 pamoja na vifaa mbalimbali zilichangwa
na wadau hao kwa ajili ya kufanikisha tamasha hilo ambalo linatarajia
kufanyika tarehe 30/10/2011 – 4/11/2011 katika viwanja wa Karimjee
jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake
na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa kumuwezesha mwanamke kunasaidia
jamii na taifa kupunguza umaskini wa kipato cha watu hivyo inachangia
utekelezaji wa lengo la kwanza katika malengo ya millennia linalohusu
kupunguza umaskini kwa nusu ifikapo mwaka 2015.
“Mimi binafsi nimeshiriki mara kadhaa katia shughuli za kuendeleza
ujasiriamali kwa wanawake na nimejionea jinsi wanawake wakiwemo
wenye ulemavu na waishio na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wanavyotambua
umuhimu wa kuongeza kasi katika juhudi za kuleta maendeleo kwao
na kwa kila Mtanzania. Napenda kuwahakikishia kuwa jukwaa la MOWE
ni mfano bora sana wa kuendeleza wanawake wajasiriamali”, alisema
Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwataka viongozi wa makampuni waliohudhuria
katika hafla hiyo kupanga utaratibu wa kudumu wa kuchangia tamasha
hilo ambalo Shirika la Kazi Duniani (ILO) limekuwa likisimamia
kwa muda mrefu ili ILO itakapomaliza muda wake wa kusimamia tamasha
hilo liendelee kufanyika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa ILO nchini Alexio Musindo alisema
kuwa wameshafadhili matamasha manne kama hayo na wataendelea kufadhili
mengine kwani ukimuunga mkono mwanamke utakuwa umemuandalia maisha
mazuri ya hapo baadaye pia wanawake wajasiriamali wamekuwa mstari
wa mbele katika kuhakikisha kuwa wanapambana na umaskini na hivyo
kuinua kipato cha familia zao.
Musindo alisema, “Moja ya malengo ya ILO ni kutoa nafsi kwa wanawake
na wanaume ili waweze kufanya kazi kubwa, za kati na ndogo ambazo
zitawaongezea kipato katika mazingira ya uhuru, usawa na ubinadamu
kwani ujasiriamali ni chanzo kikubwa cha mapato, ajira na uzalishaji
mali”.
Aliendelea kusema kuwa tamasha hilo litawakusanya maelfu ya wanawake
wajasiriamali ambao wataweza kubadilishana mawazo, ujuzi pamoja
na kujifunza teknolojia mbalimbali za kuzalisha bidhaa zao pia
wataweza kupata masoko ya kuuza bidhaa zao na kujipatia fedha.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya MOWE Elihaika Mrema alisema kuwa
tukio hilo limekuwa likiadhimishwa hapa nchini tangu mwaka 2006
baada ya kujifunza kutoka nchi za Ethiopia mwaka 2004 na Zambia
mwaka 2005.
Mrema alisema kuwa sababu za kuanzishwa kwa MOWE ni baada ya
kutambua changamoto zilizokuwa zinawakabili wajasiriamali wanawake
wakiwemo wenye ulemavu na waishio na VVU. Changamoto hizo ni uwezo
mdogo wa kuyafikia masoko ya uhakika, ukosefu wa mitaji, maeneo
bora ya kuzalishia bidhaa au kufanyia biashara, kushindwa kumudu
gharama za utangazaji wa bidhaa au huduma wazalishazo na ugumu
wa upatikanaji wa habari.
“Matokeo ya MOWE ni kutangaza kwa vitendo mafanikio ya maendeleo
ya kiuchumi na kijamii yaliyotokana na juhudi za wanawake wa rika
zote, mijini na vijijini wakiwemo wenye ulemavu na waishio na
VVU”, alisema Mrema.
Tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka kwa mwaka huu linaratibiwa
na Taasisi ya WAMA na litakusanya wadau kutoka mikoa yote nchini
hasa wanawake wa rika zote wakiwemo wenye ulemavu na waishio na
VVU huku kauli mbiu ikiwa ni “miaka 50 wanawake wajasiriamali
tunaweza tutumie Fursa”.
.
|