..FOUNDATION NEWS

Wake wa Marais barani Afrika wametakiwa kuwaelimisha wanawake ili waweze kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Januari 31 2011

Na Anna Nkinda – Addis Ababa, Ethiopia

Wake wa Marais barani Afrika wametakiwa kuwaelimisha wanawake ili waweze kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto jambo ambalo litaweza kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Wito huo umetolewa leo na mke wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban- Ki moon mama Yoo-Soon- Taek wakati akifungua mkutano mkuu wa wake za Marais Barani Africa (OAFLA) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya umoja wa Africa (AU).

Mama Yoo- Soon Taek alisema kuwa vifo vya watoto wachanga vinavyotokana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto hivi sasa vimeongezeka hivyo basi ni jambo jema kama wataweza kufanya kazi kwa pamoja ili kupunguza vifo hivyo.

“Nafasi yenu katika jamii ni kubwa sana hivyo basi kwa kushirikiana na wananchi mnaweza kupunguza vifo hivyo na kuhakikisha kuwa hakuna mtoto ambaye atazaliwa huku akiwa amepata maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kwani mkiamua kufanya hivyo hakika mtaweza”, alisema.

Pia aliwataka wake hao wa marais kuwawezesha wanawake ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya uchumi jambo ambalo litawasaidia kujikwamua kimaisha na hivyo kutokuwa katika mazingira ambayo yatawasababishia kupata maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI.

Akitoa mada katika mkutano huo Dr. Sheila Sisulu ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) alisema kuwa shirika hilo limekuwa likinunua chakula mashambani ambacho kwa asilimia 70 kinazalishwa na wanawake lakini jambo la kushangaza ni kuwa wanawake hao baada ya kuuza chakula hicho wanakinunua tena kwa bei kubwa.

Aliendelea kusema kuwa jambo wanalolifanya hivi sasa ni kuwawezesha wanawake wakulima ili waweze kuuza vyakula wanavyovizalisha katika shirika hilo kwani watalipwa fedha nyingi ambazo zitawasaidia kuinua kipato cha familia zao.
Dr. Sisulu alisema, “Ninawaomba muweze kuwawezesha wanawake ili waweze kununua vyakula na kuuza katika shirika letu kwani watalipwa pesa nyingi ambazo zitawasaidia kusomesha watoto wao na kutunza familia zao kwakuwa hakuna ushindani wa kibiashara na soko ni kubwa”.

“Tunataka kutoa pesa katika mifuko ya wanawake kwani wanawake wanapokuwa na pesa watoto watasoma na kupata chakula na hivyo kupunguza umaskini ndani ya familia tofauti na wanaume”.

Alimalizia kwa kusema kuwa ukimsomesha mtoto wa kike utakuwa umeelimisha familia nzima pia mtoto huyo atachelewa kuolewa na hivyo kupunguza ndoa za utotoni.

Naye Rais wa umoja huo mke wa waziri mkuu wa Ethiopia Mama Azeb Zenawi alisema kuwa hivi sasa umoja huo unakabiliwa na changamoto kubwa ya kupambana na ugonjwa wa UKIMWI kwa wanawake jambo ambalo linasababisha vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga.

Changamoto zingine ni upungufu wa vitendea kazi vya kutosha pamoja na fedha za kutosha ambazo zitawasaidia wanachama wa umoja huo kuwawezesha wanawake katika nchi wanazotoka.
Mkutano huo ambao umemalizika leo ulihudhuriwa na wake wa marais kutoka nchi 19 akiwemo Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Salma Kikwete.

 

Site Search