Mwenyekiti wa Wama Mama Salma Kikwete awagawia salio Saccos ya Seuma - Juni 16,2011
By Mwanakombo Jumaa
Wanawake nchini wameaswa kutoogopa kusoma na kutokuwa wanyonge katika harakati zao za kujiletea maendeleo na kuwawezesha kupata nafasi mbalimbali za uongozi nchini..
Rai hiyo imetolewa Juni 15, 2011 na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete katika sherehe ya kufunga mwaka 2010-2011 na kufungua mwaka 2011-2012 na kukabidhi gawio la kikundi cha SEUMA SACCOS –A- kilichopo Segerea wilaya ya Ilala mkoani Dar Es Salaam .
“Wanawake wenzangu katika dunia ya leo sio dunia ya mwanamke kuwa mnyonge, changamoto kwenu tujitoe wanawake katika masuala mbalimbali ili tujitegemee tusonge mbele na kuwa chachu ya maendeleo na kuacha kulalamika” alisema Mama Salma.
Mama Salma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) amewashauri wanakikundi hao kutokata tamaa kwenye suala la ushiriki wa wanachama wakiume kuonekana wachache na badala yake ni vizuri kuwaonyesha kuwa wanawake wanaweza kusongambele na kujiletea maendeleo yao.
Aidha na sherehe za kufunga na kufungua mwaka zilishuhudia hafla ya kugawa salio la Tsh Milioni 18 kwa kipindi cha mwaka mmoja wa kikundi hicho.
Katika risala yao ya kumkaribisha mgeni rasmi SEUMA SACCOS A wamesema kikundi chao kimeweza kupatiwa mafunzo mbalimbali na Shirika la Care International kwa mpango wa Ongeza Akiba na wamenunua hisa kwa ajili ya kukopeshana na kujiwekea akiba kwa ajili ya kusaidiana matatitzo mabalimbali ya kijamii.
SEUMA SACCOS A- wameweza kuanzisha kikundi chengine cha SEUMA B na tayari wamekwisha gawana gawio la kwanza na linaendelea vizuri, pamoja na kutoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Tsh 250.000 /= kwa waathirika wa mabomu ya Gongo la mboto na kumhudumia kimasomo mtoto yatima Mariam Yahya .
Kikundi cha SEUMA A (Segerea Ugombolwa Machimbo) kilianzishwa tarehe 29/01/2010 na kilisajiliwa tarehe 6/3/2010 kikiwa na wanachama thelathini kati yao wanaume sita na wanawake 24.
|