..FOUNDATION NEWS

WAMA yasisitiza umuhimu wa uboreshaji afya Na Elimu Mkoani Pemba Mei 14, 2010

Na Philomena Marijani

Taasisi ya WAMA imesisitiza umuhimu wa uboreshaji afya na Elimu katika Ziara yake ya Maendeleo Mkoani Pemba Alhamisi Mei 13 2010. Akikabidhi msaada wa vifaa vya hospitali katika Hospitali ya Chakechake iliyoko Pemba Mwenyekiti wa WAMA Mhe. Mama Salma Kikwete alisema kuwa vifo vya akina mama na watoto bado ni tatizo kubwa visiwani. Alisema kuwa juhudi za dhati bado zinahitajika ili kuhakikisha kuwa wakina mama wanajifungua salama.

Aidha aliwapongeza viongozi kwa kujiweka malengo ya kupunguza vifo vya mama wajawazito kutoka 377 kati ya vizazi hai 100,000, hadi kufikia 251 na kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka 5 kutoka 101 kati ya watoto 1000 hadi kufikia 71 kwa mwaka huu.

Vifaa vilivyotolewa ni vifaa vya kujifungulia (Delivery Kit) (01), vifaa vya operesheni ndogo (caesarean kit)(01) na huwa vinadawa ya kusafishia (self sterilization), Kifaa cha kuvutia uchafu kwa watoto wanaozaliwa (Sunction pump) kimoja (01), Toroli la kubebea vifaa vya huduma wodini (Dressing Troley) (01), Mzani wa watoto (Infant Scale), Vitanda vya hospitali (2) , Magodoro (2), na Mashuka (4).


Mwenyekiti wa WAMA pia alitembelea Kituo cha Kazi za Amali-Vitongoji, ambapo pia aliweza kuongea na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Fidel Castro ambapo alielezea umuhimu wa kazi za kituo hicho kwa ajira za vijana . Kituo cha Amali kinatoa mafunzo ya ufundi ya umeme, kompyuta, useremala, Magari, uashi, na bomba.


Katika hotuba yake kwa Wanafunzi aliwasihi wawe makini na masomo yao na waepuke na mambo yote yanaweza kuwaangusha kitaaluma.

“Jiwekeeni malengo makubwa ya kitaaluma, ili msiishie kufuzu katika ngazi hii ya mafunzo, na sekondari bali, mfaulu na mpate sifa zitakazowawezesha kuendelea na kozi za mafunzo zaidi kwa ngazi ya elimu ya juu na hata ngazi ya vyuo vikuu.” Alisema Mama Salma.

Site Search