Mke wa Rais,
Mama Salma Kikwete amezitaka taasisi za fedha duniani kutoogopa
kuwakopesha wanawake kwani wamekuwa na sifa njema ya kurejesha
mikopo kuliko wanaume
Na Gloria Tesha, Beijing, China .
Mama Salma aliyasema hayo juzi mjini hapa alipokuwa
akitoa salamu kwa ufupi katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa
wa Wanawake (Global Summit of Women-GSW) uliofanyika katika
ukumbi wa Great Hall of People.
“Ukiwakopesha wanawake, una uhakika wa mkopo
kurejeshwa maana anaelewa changamoto zinazomkabili na majukumu
aliyonayo katika familia na jamii kwa ujumla, taasisi za fedha
wasiogope kuwakopesha wanawake,” alisema Mama Salma.
Katika salamu zake hizo, Mama Salma akiwa mke
pekee wa Rais kati wake kadhaa wa marais wa Afrika walioalikwa
katika mkutano huo ambao hawajafika mpaka jana, alisema siku
zote wanawake wamekuwa hodari kurejesha mikopo na kutekeleza
lengo la mikopo kwa wakati hivyo hakuna sababu kwa taasisi za
kifedha za kimataifa na katika kila taifa kuogopa kuwakopesha.

Akitolea mfano kwa nchini Tanzania, Mama Salma
bila kufafanua zaidi, alisema takwimu zinaonesha kuwa, kati
ya wanaume na wanawake wanaokopeshwa fedha kwa ajili ya biashara
na miradi mbalimbali, wanawake wamekuwa wepesi kurejesha ingawa
imekuwa vigumu kuwakopesha kutokana na hofu ambayo haina umuhimu.
Alisema nchi yoyote inayotaka kufanikiwa kiuchumi,
lazima imuweke mwanamke mbele kwa kuwa majukumu yake ni mengi
na endapo akipewa mwelekeo, anaweza kuyashughulikia na kuyapatia
ufumbuzi.
“Wanawake tulio hapa tunawawakilisha wanawake
wenzetu kote duniani, na kwa bahati sisi hapa tumekuwa
katika nafasi za juuu kuliko pengine wenzetu walio wengi, tunapokuwa
hapa tujifunze kwa wenzetu waliofanikiwa zaidi ili tunaporejea
makwetu tuhakikishe tunamuinua mwananmke mwenzetu kutoka chini
hadi afike juu,” alisisitiza Mke wa Rais.
Katika ufunguzi huo uliofanywa kwa viongozi
kutoa salamu fupi, uliwashirikisha pia Makamu wa Rais wa Vietnam,
Nguyen Thi Doan, Waziri wa Wanawake wa Chile, Carolina Schmidt,
Maud Olofsson, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Sweden,
Rais wa GSW na Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanawake wote wa
China (ACWT).
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Vietnam, Thi Doan, alisema
akiwa mwanamke, anajivunia kuwa kiongozi kutokana na sera za
taifa lake kumuinua mwanamke na kuwataka wanawake kuthubutu
kuweza pale wanapopewa nafasi za uongozi, biashara na uchumi
.
Aidha pia alisema kutokana na kuwa kundi kubwa
linalosakamwa na majukumu pamoja na hatari za maradhi, alisema
mataifa hayana budi kuweka mazingira mazuri kuwezesha wanawake
kufungua miradi na kukuza kipato chao.
|