Mke wa Rais
na Mwenyekiti wa WAMA atia fora na kungara katika Mkutano wa
Kimataifa wa Wanawake, Beijing – China , Mei
21 2010
Na Gloria Tesha, Beijing
MKE wa Rais, Mama Salma Kikwete ametia fora
na kung'ara katika Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake unaoendelea
mjini hapa kutokana na hotuba yake kugusa maisha ya wanawake
kiasi cha kusababisha kila mtu kutaka apige nae picha.
Hali hiyo ilijitokeza mara baada ya kutoa hotuba
fupi ya salamu katika ufunguzi wa mkutano huo katika ukumbi
wa Great Hall of The People mjini hapa juzi ambapo halfa hiyo
ilipofungwa na wageni kuelekezwa ukumbi mwingine wa Banquet
kwa ajili ya burudani, alishindwa kutoka moja kwa moja kutokana
na watu kumsonga wakitaka kila mmoja kupiga nae picha.
Kazi ilikuwa ngumu kwa maofisa wa usalama na
baadhi ya watu waliozungumza na mwandishi wa habari hizi walieleza
kuwa, wameguswa na hotuba yake ambayo imekuwa tofauti na hotuba
nyingine kutokana na kuzungumza mambo katika hali halisi.

Marilyn Johnson, Makamu wa Rais wa kampuni
ya IBM kutoka Marekani, alisema kutokana na hotuba hiyo ya Mama
Salma aliyoitoa kwa Kiswahili na kutafririwa wa kiingereza,
anatamani kupata mwaliko kuja Tanzania siku moja ili kuona namna
Watanzania hasa wanawake wanavyoweza kutumia nafasi ya kuwa
na mke wa rais kama huyo, kuinuka kiuchumi.
“Akinialika kupitia taasisi yake (WAMA) nitakuja
Tanzania wakati mmoja, nimevutiwa na mazungumzo yake, yamenigusa,”
alisema Johnson.
Miongoni mwa wanawake waliogombea nafasi ya
kupiga picha na mke wa rais ni kutoka nchini Mongolia ambao
walipohojiwa walisema ni mke pekee wa rais wa Afrika, ambaye
kupitia taasisi yake, ameonesha kuwajali wanawake na ni mfano
wa kuigwa.
Katika hotuba yake mbali na kutaka wanawake
wawezeshwe na taasisi za kifedha, pia alitaka mataifa yakubali
kuwa mwanamke anaweza, anapowezeshwa na kupewa nafasi hivyo
kuyataka yathamini mwanamke.
Mama Salma alisema mwanamke ana majukumu mengi,
ni mama, mlezi wa watoto wadogo na mtoto mkubwa (mume) lakini
pia ni kiongozi na mzazi.
“Pamoja na yote hayo, mwanamke anaweza kutekeleza
majukumu yote anayopewa, haijalishi yote haya, hivyo wanawake
wanaweza,” alisistiza Mama Salma na kushangiliwa.
Leo mke wa rais anatarajiwa kutoa mada fupi
kuhusu mafanikio ya WAMA na nafasi yake kama mke wa rais (kiongozi)
katika kuwasaidia wanawake kabla ya sherehe ya kufunga mkutano.
|