Watanzania
watakiwa na kampeni za siasa na kujihusisha na shughuli za maendeleo
Na Anna Nkinda – Mkuranga, 08/05/2011
Wananchi wilayani Mkuranga wametakiwa kuachana na itikadi za kisiasa
katika shughuli za maendeleo kwani suala la maendeleo linamgusa
kila mtu na si chama cha kisiasa.
Wito huo umetolewa jana na mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati
akifungua Chama Cha kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) ya Salma Kikwete
iliyopo kijiji cha Hoyoyo wilayani Mkuranga katika mkoa wa Pwani.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) alisema kuwa hivi sasa wananchi wanatakiwa kuachana
na masuala ya kampeni za uchaguzi na kujishughulisha zaidi katika
mambo ya maendeleo pasipo kubaguana kwani wakati wa kampeni ulishapita
mwaka 2010
“Nataka mfahamu kuwa SACCOS ni chombo cha kujiletea maendeleo
hata kama chimbuko lake ni ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),wewe
kama utakataa kujiunga na SACCOS hii kwa madai kuwa mbona ina
jina la mama Kikwete, mbona ilifunguliwa na Mke wa Rais shauri
lako wenzako watajiunga, watapata pesa na kuzifanyia shughuli
za maendeleo wewe utabaki kama ulivyo,”alisema Mama Kikwete.
Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwaasa wanachama wa SACCOS hiyo
kuitumia vizuri mikopo watakayoipata katika shughuli za maendeleo
kama kuongeza mitaji ya biashara, kuboresha mashamba na makazi
na kuboresha maisha ya familia kwani kwa kufanya hivyo watayaona
manufaa ya SACCOS.
Mama Kikwete alionya, “Mkitumia vibaya mikopo watakayoipata mtashidwa
kuboresha maisha yenu na wakati mwingine kushindwa kurudisha fedha
mlizozikopa ambazo wanachama wengine wanazihitaji. Na hatimaye
SACCOS yenu kufilisika.”
Aliwaomba wataalamu wa biashara wawe karibu na wananchi ili kuwapa
elimu ya kuendesha biashara na hatimaye biashara hizo ziweze kuzalisha
faida na hivyo kuwapa wepesi wa kurudisha fedha walizokopa.
Wanachama wengi wa SACCOS hiyo wanategemea kilimo, lakini Mama
Kikwete aliwashauri wakishiriki katika biashara ndogondogo ambazo
zitawasaidia kupata mahitaji muhimu ya familia ili kuongeza kipato
kinachopatikana kutokana na kilimo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini Adam Malima alisisitiza
kuwa jambo kubwa wanaloliangalia hivi sasa ni jinsi ya kumkomboa
mwananchi kutoka katika hali ya maisha duni na kuishi maisha ambayo
yatampatia kipato kila siku na hivyo kujikwamua na umaskini.
“Ninakupongeza sana kwa jitihada zako unazozifanya za kuwakomboa
wananchi hasa waishio vijijini nasi tunakuunga mkono kwa kuwahimiza
wananchi waone umuhimu wa kujiunga na vikundi mbalimbali vya maendeleo
kwani kwa kufanya hivyo watakopa na kupata pesa ambazo zitawasaidia
kufanya mambo ya maendeleo,”alisema Malima.
Akielezea historia ya SACCOS hiyo Somoye Kilimile ambaye ni Mweka
hazina alisema kuwa ilitokana na wazo la Mama Kikwete la kutumia
sehemu ya shamba lake kama kituo cha mafunzo ya kilimo na ufugaji
alichokizindua tahere 23/02/2008 kama shamba darasa kwa ajili
ya kujifunza uzalishaji wa zao la pilipili baridi (paprika), migomba,
miembe ya kisasa na ufugaji wa kuku wa kienyeji chini ya usimamizi
wa taasisi ya WAMA, viongozi wa kijiji cha Hoyoyo, wilaya ya Mkuranga
na Wizara ya Kilimo.
Alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni upungufu wa
mtaji kwani lengo lao ni kupata mtaji wa zaidi ya shilingi milioni
100 na mtaji walionao ni shilingi milioni tatu na laki nane, ukosefu
wa fedha kwa ajili ya kuendeshea ofisi ikiwa ni pamoja na gharama
za kukodi, mishahara na shajala na ukosefu wa eneo kwa ajili ya
kujenga ofisi ya kudumu.
“Mipango ya baadaye tuliyonayo ni kutafuta shamba kwa ajili ya
kuanzisha kilimo cha mazao ya biashara na chakula pamoja na ufugaji
kutafuta eneo na kujenga jengo litakalotumia kwa shughuli za ofisi
na kitega uchumi na kuanzisha miradi midogomidogo na ya kati kwa
ajili ya kutoa ajira kwa wanachama”, alisema Kilimile.
SACCOS hiyo ilianzishwa tarehe 12/10/2009 ina wanachama 103
kati ya hao 65 ni wanawake na 38 ni wanaume.
Zaidi ya shilingi milioni 51 zilipatikana katika harambee iliyoendana
sambamba na ufunguzi wa SACCOS hiyo ambapo Taasisi ya WAMA iliichangia
shilingi milinoni tatu na laki nane.
|