..NEWS & EVENTS

Wanawake 80,000 wanaweza kupoteza maisha na milioni mbili na nusu kupata ulemavu ikiwa juhudi za dhati hazitafanyika ili kutatua tatizo la vifo vya kina mama wajawazito na watoto

 Missenyi – Kagera Julai 28, 2009

Wanawake 80,000 wanaweza kupoteza maisha kati ya mwaka 2008 mpaka 2015 pia wanawake milioni mbili na nusu wanaweza kupata matatizo ya ulemavu ikiwa juhudi za dhati hazitachukuliwa ili kuweza kukabiliana na tatizo la vifo vya kina mama wajawazito na watoto hapa nchini.

 Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wananchi wa Bunazi mara baada ya kukabidhi vitanda viwili vya kujifungulia katika kituo cha Afya Bunazi kinachomilikiwa na Halmashauri ya wilaya ya Missenyi.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa kwa bahati mbaya sana idadi ya vifo vya kina mama hapa nchini ipo juu kwani inakadiriwa kuwa mwanamke mmoja hufariki kila baada ya saa moja kwa siku kutokana na matatizo ya uzazi.

"Idadi hii ni kubwa sana haswa kwa sababu vifo hivi vingeweza kuepukika kwani vinatokana na ushiriki na ushirikishwaji finyu wa jamii katika masuala ya afya, ugumu wa kufika vituo vya huduma ya afya mapema, uelewa mdogo juu ya masuala ya uzazi na afya ya mama na mtoto, kuchelewa kufanya maamuzi ya kwenda Hospitali mara uchungu unapoanza", alisema Mama Kikwete.

 Alizitaja sababu zingine zinazosababisha vifo hivyo kuwa ni mila na desturi potofu zinazoathiri afya za kina mama kama ukeketaji, kukatazwa kula aina fulani ya vyakula, utumikishwaji wa wanawake hususani wakati wa ujauzito na vipigo kwa wanawake wakati wakiwa wajawazito .

Kwa upande wa vifo wa watoto wadogo Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema kuwa kwa wastani watoto sita hufariki kila siku kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya kama jamii ikijipanga vizuri inaweza kupunguza vifi hivi kwa kiasi kikubwa sana.

Aisoma taarifa ya kituo hicho Daktari Mfawidhi Levitas Rwazo alisema kuwa kituo kinatoa huduma za tiba na wanapokea wagonjwa wa nje 90 na wa kulazwa 12 kwa siku. Pia wanatoa tiba ya kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa wa UKIMWI (CTC) ambapo wagonjwa 253 wanahudumiwa na kati ya hao wagonjwa 135 sawa na asilimia 53.4 wanatumia dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi.

Huduma zingine zinazotolewa kituoni hapo ni kinga, elimu ya afya na utoaji wa rufaa kwa wagonjwa kwa wastani mama mjamzito na mtoto mmoja hupewa rufaa kila siku ya kwenda katika Hospitali za Mugana, Mkoa na Kiwanda cha Sukari Kagera kutokana na upungufu wa damu .

"Upimaji wa hiari (VCT) kwani tangu kuanza kwa kampeni ya upimaji kwa hiari jumla ya watu 17983 wamepima katika kituo hicho na waliokutwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa UKIMWI ni 648 sawa na asilimia 3.6 ikilinganisha na kiwango cha asilimia 5.9 katika wilaya ya Missenyi".

"Kwa mwaka 2008 jumla ya wagonjwa 834 walipatiwa huduma ya kuzuia maambukizi toka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto (PMTCT) na kati ya hao 25 walikutwa na maambukizi sawa na asilimia 2.9", alisema Dk. Rwazo.

Aliendelea kusema kuwa kituo hicho kinakabiliwa na uchakavu na upungufu wa majengo ya kutolea huduma hasa wodi za wagonjwa na nyumba za kuishi, upungufu wa watumishi wenye ujuzi, upungufu wa chumba cha upasuaji pamoja na vifaa na uchakavu wa gari la kituo.

Kutokana na ombi la kituo hicho la vifaa vya kutunzia damu (jokofu na mzani wa kupimia damu) kwani kituo kupokea wagonjwa wengi wenye upungufu wa damu hasa kina mama wajawazito na watoto pia kwa kuwa kipo karibu na barabara kuu itokayo Uganda kwenda Bukoba hupokea majeruhi wengi wa ajali za barabarani ambao hupungukiwa damu. Mama Salma Kikwete aliwaahidi kuwaletea jokofu hilo.

Kituo hicho cha Afya kilianzishwa kama zahanati mwaka 1920 na kupandishwa hadhi kuwa kituo cha Afya mwaka 1970 kinahudumia wakazi wapatao 17,606 wa kata ya Kassambya na kina wodi ya watoto, wazazi, wanaume na wanawake.

Mama Kikwete amemaliza jana ziara ya kikazi ya siku tatu katika mkoa wa Kagera yenye lengo la kuchangia juhudi za kupunguza vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi kwa kutoa vifaa vya huduma ya afya ya uzazi, hususan katika wodi za wazazi. Kuhamasisha juhudi za maendeleo kwa wanawake kupitia vikundi vya SACCOS na benki za vijijini- VICOBA.

Kuhamasisha juhudi za kupunguza matukio ya mimba na utoro mashuleni, kuhamasisha vikundi vya SACCOS na benki za vijijini- VICOBA na kuhamasisha juhudi za kupunguza matukio ya mimba na utoro mashuleni.

Site Search