Wanawake mkoani Morogoro watakiwa kuwa mstari wa mbele katika shughuli za maendeleo
Na Anna Nkinda - Maelezo, Morogoro - 20/10/2009
Wanawake mkoani Morogoro wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kujihusisha na shughuli za maendeleo ili waweze kujikomboa kiuchumi kwani kuanzia ngazi ya familia wao ndio wazalishaji wakubwa ukilinganisha na wanaume.
Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wakina mama wa kikundi cha kilimo cha umwagiliaji cha umoja ni nguvu kilichopo kijiji cha Sinyaulime kata ya Ngerengere wilaya ya Morogoro.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliendelea kusema kuwa mradi huo ni wa muhimu sana kwa wakati huu ambao serikali inatilia mkao suala la kilimo kupitia kauli mbiu ya kilimo kwanza hivyo basi ni wajibu wa kila mmoja kutekeleza kauli mbiu hiyo kwa vitendo.
"Ninawashauri muwatumie vizuri wataalamu wa kilimo na kuutumia ushauri wao katika kila hatua ya kazi zenu msisubiri hadi mazao yanaposhambuliwa na wadudu ndiyo mnawatafuta kwa kufanya hivyo mtazalisha mazao mengi na ya kisasa zaidi", alisema Mama Kikwete.
Mama Kikwete pia aliwakumbusha viongozi wa wilaya hiyo kwamba katika mipango ya maendeleo wasisahau kuweka mipango ya makusudi itakayolenga kutatua changamoto zinazowakabili wanawake katika shughuli zao za maendeleo ikiwemo kilimo cha umwagiliajia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi hicho Josephine Pangalugobe alisema kuwa shughuli zinazofanywa na kikundi hicho ni kilimo cha mboga mboga ambacho kinaendeshwa katika bustani yenye ukubwa wa hekari sita lakini hadi sasa eneo wanalolitumia ni hekari moja na nusu na wateja wao wakubwa ni wanakijiji wa Sinyaulime pamoja na wakazi wa Ngerengere.
Pangalugobe aliendelea kusema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukame uliojitokeza miezi ya hivi karibuni na uhaba wa mtaji kikundi kina Akaunti benki yenye fedha kiasi cha shilingi 150,000/=.
"Katika kukabiliana na changamoto hizo kikundi kinampango wa kuchimba kisima ambacho kitasaidia kukabiliana na tatizo la ukame ili kutuwezesha kulima mbogamboga kwa muda wa mwaka mzima", alisema.
Kikundi hicho pia kina mradi wa ufugaji wa kuku wa asili, mradi wa ufyatuaji wa matofali hadi sasa wanajumla ya matofali 20,000.
Akisoma taarifa ya wilaya hiyo Mkuu wa wilaya Said Mwambungu alisema kuwa Halmashauri inajumla ya vikundi 98 vya wanawake vinavyojishughulisha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Aliendelea kusema kuwa wanawake wamekuwa wakijiunga katika vikundi vingine mchanganyiko mfano katika programu ya Benki jamii vijijini (VICOBA) Halmashauri ina vikundi 36 na idadi ya wanavikundi ni 997 kati yao 478 ni wanawake wanaoshiriki katika Benki hizo.
Kuhusiana na suala la wanawake kujiunga katika vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) Mwambungu alisema kuwa hadi sasa kuna jumla ya wanachama 4,555 kati yao 1,512 ni wanawake vilevile wanawake wa wilaya hiyo wamekuwa wakijishughulisha katika shughuli za kilimo.
Mwambungu alisema, "Changamoto kubwa inayoikabili wilaya hii ni mwamko mdogo wa wanawake kujiunga katika vikundi vya kiuchumi mfano vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS), Benki jamii (VICOBA) hata hivyo tunaendelea kuwahamasisha wanawake kujiunga katika vikundi hivyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali".
Taasisi ya WAMA ilikichangia kikundi hicho shilingi milioni moja ili ziweze kutumika katika kuinua mtaji na kufanya shughuli za maendeleo.
Kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2007 kikiwa na wanachama 26 huku lengo lao likiwa ni kuwawezesha wanakikundi kufanya kazi kwa ushirikiano na kubadilishana ujuzi na maarifa , kuongeza kipato kwa wanachama wake ili waweze kupunguza kiwango cha umaskini kwa kuwawezesha walengwa kupata mahitaji yao ya muhimu pamoja na kuongeza mtaji wa kuendeleza kikundi.
Wakati huo huo Mama Kikwete alitembelea zahanati ya Mvuha iliyopo wilayani humo na kuwapatia kitanda cha kujifungulia kimoja, vitanda vya Hospitali viwili, magodoro mawili, mashuka manne, mashine ya kupimia mapigo ya moyo (BP Machine) moja, mzani wa kupimia watu wazima mmoja mabox ya sindano mawili na Stethoscope moja.
|