Jamii
yatakiwa kuwaacha watoto wa kike wasome, October 14, 2011
Na Anna Nkinda – Maelezo
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ameitaka jamii nchini kutowaoza
watoto wa kike wakiwa masomoni kwani ng’ombe wanaolipwa wazazi
kama mahali hawana faida ukilinganisha na elimu ambayo angeipata
mtoto huyo.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake
na Maendeleo (WAMA) aliyasema hayo jana wakati akiongea na wakazi
wa wilaya ya Tarime mkoani mara kwenye sherehe za kilele za wiki
ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na maadhimisho ya miaka 50
ya Uhuru yaliyofanyika wilayani humo.
Alisema kuwa ni jambo la muhimu kwa wazazi na jamii kuwaruhusu
na kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanasoma na hawakatishi masomo
yao kwa kuwaoza au kupata ujauzito jambo ambalo linawafanya wanafunzi
hao kutotimiza ndoto zao kwa kuwaharibia maisha yao kwani ukimuendeleza
mtoto wa kike ni sawa na kuiendeleza jamii nzima.
Mama Kikwete alisema, “ Hivi sasa kuna tatizo kubwa la watoto
wa kike kukatiza masomo baada ya kupata ujauzito na jambo la kusikitisha
ni jinsi mzazi anavyoshirikiana na kijana aliyempa ujamzito binti
yake kuharibu ushahidi na hivyo kufanya sheria kutochukua mkondo
wake kwa kufanya hivyo mnasababisha watoto wasiwe waoga wa kufanya
mapenzi kabla ya wakati na tazizo la mimba za utotoni kuwa sugu”.
Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwataka wanaume kuwasaidia wake
zao kazi mbalimbali wanazozifanya hasa katika ulezi wa familia
kwani ulezi wa mtoto ni wa wazazi wote wawili na jamii nzima inayowazunguka
.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo John Henjewele alisema kuwa
pamoja na jitihada za halmashauri kuhakikisha watoto wanapata
haki za msingi katika sekta ya elimu bado kuna tatizo kubwa la
mimba mashuleni na ndoa za utotoni.
Alisema kuwa tangu mwaka 2008 hadi 2011 wanafunzi 46 wamepata
ujauzito kati ya hao 33 ni wanafunzi washule za Sekondari na 13
ni wa shule za Msingi.
“Tatizo hili linasababishwa kwa kiasi kikubwa na mila na desturi
potofu zinazoshawishi kufanyika kwa matendo hayo katika umri mdogo.
Aidha uchukuaji wa hatua za kisheria unakatizwa na usiri uliopo
kwa wananchi, hasa wazazi kuogopa au kukataa kuwafichua wahalifu”,
alisema Henjewele.
Mama Kikwete alikuwa mkoani Mara kwa ajili ya maadhimisho ya
miaka 50 ya Uhuru na kilele cha wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT) ambayo kilele chake kilifanyika jana katika wilaya ya Tarime.
|