UWT
watakiwa kuwaenzi waasisi wa umoja huo, October 14,2011
Na Anna Nkinda – Maelezo, Tarime
Wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wametakiwa kuwa
wavumilivu, na upendo, uzalendo kwa Taifa, utayari wa kuthubutu
na kutenda walichokiazimia, kushikamana na kupeana moyo wakati
wote wa kumkabili adui ili waweze kuwaenzi waasisi wa umoja huo.
Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati
wa sherehe za kilele za wiki ya UWT na maadhimisho ya miaka 50
ya Uhuru yaliyofanyika wilayani Tarime katika mkoa wa Mara.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake
na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa waasisi wa umoja huo waliongozwa
na umoja, ujasiri, usikivu, kujiamini, kukubali majukumu, kuwa
tayari kutumwa, moyo wa kujitolea, kushikamana na kutokukata tamaa
haraka mambo ambayo yameshindwa kuenziwa na wanawake wa leo na
hivyo kutokupata mafanikio kama yale ya waasisi wao.
“Kwetu sisi Mwalimu alikuwa mtu wa pekee na muhimu sana kutokana
na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa wanawake na kwa kutambua
siri ya nguvu kubwa za wanawake katika kufanikisha mapambano ya
kuikomboa nchi yetu pia aliwaunganisha wanawake kwa kuanzisha
UWT chini ya TANU chombo ambacho ni tuzo kwetu ya kutambua mchango
wetu kwenye mapambano ya kudai uhuru wa nchi yetu na kwa ujenzi
wa Taifa”.
“Nafarijika kuwa wanawake tunaweza, si jana wala juzi bali uwezo
wetu ulianza zaidi ya miaka 50 iliyopita na bado tunaendelea jambo
la muhimu ni kufanya kazi kwa bidii, upendo na moyo wa kujitolea
kama ilivyo kawaida yetu tukifanya hivyo tutakuwa tumetetea maslahi
yetu na jamii nzima , kwa maana mama ndiye mlezi wa familia”,
alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alizitaja changamoto inazowakabili wanawake
ambazo zinaakisi sura na majukumu ya mwanake katika jamii na hivyo
kuiomba Serikali kuzitatua kuwa ni mwanamke ni shina la uhai wa
jamii, kielelezo cha uhai wa Taifa, uhai wa Chama, mama wa jamii,
anamiliki jamii, anawasiliana na jamii, anailea jamii na anahamasisha
jamii.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa umoja huo Amina Makillagi alisema
kuwa kila mwaka UWT hufanya maadhimisho ya Umoja huo, sherehe
ambazo hufanyika kati ya mwezi Septemba na Oktoba ambapo katika
wiki hiyo wanawake hukutana nchi nzima kukumbuka siku ambayo umoja
huo ulianzishwa Novemba 2, 1978, kutathini mafanikio waliyoyapata
wanawake wa Tanzania na changamoto mbalimbali zinazowakabili.
“Tuliamua kuyafanya maadhimisho haya ya UWT ya mwaka huu wa 2011
yawe maalum kwa ajili ya kutupatia fursa maalum ya kuadhimisha
miaka 50 ya Uhuru, kumkumbuka na kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu
Nyerere kwa kuanzisha UWT na kwa kukubali kuilea , kazi aliyoifanya
hadi mwisho wa uhai wake”, alisema.
Aliyataja Mafanikio waliyoyapata tangu kupatikana kwa uhuru
ni wanawake kushiriki kwenye siasa na kupiga kura wakati wa uchaguzi,
ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za uzalishaji mali, mtoto
wa kike anapata fursa ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume,
kupungua kwa mila zinazowakandamiza wanawake,kuongezeka kwa upatikana
wa afya ya mama na mtoto.
Mafanikio mengine ni kurekebishwa kwa sheria zinazowakandamiza
wanawake na watoto, kuimarika kwa usawa wa jinsia na uwezeshaji
wanawake,wanawake kutotumika kama nguvu kazi ya uzalishaji.
Makillagi alisema, “Matatizo yanayowakabili wanawake hivi sasa
ni kuendelea kuwepo sheria zinazowakandamiza wanawake na watoto,
tatizo la mimba za utotoni na wanafunzi, upatikanaji mdogo wa
maji safi na salama na umuhimu wa kuendelea kudumisha amani na
utulivu nchini mwetu”.
Katibu Mkuu huyo wa UWT aliiomba Serikali kuchukua tahadhari
na hatua za makusudi ili kuhakikisha kuwa amani na utulivu uliodumu
nchini tokea kupatikana kwa Uhuru, unalindwa kwa gharama zote
ili Tanzania iendelee kuwa kisima cha Amani na Utulivu.
Katika maadhimisho hayo tuzo mbalimbali zilitolewa kwa waasisi
wa umoja huo akiwemo mama Maria Nyerere, Fatuma Karume, Hayati
Bibi Titi Mohamed, Hayati Mama Sophia Kawawa, Anna Abdallah, Lea
Lupembe, Dk. Msimu Abdulrahhman, Kate Kamba, , Bibi Raya wa Zanzibar
na Mama Salma Kikwete kutokana na jitihada zake za kufanya kazi
na kuisaidia jumuia hiyo.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ambayo inalenga kuwapa wanawake
fursa ya kutathimini maendeleo yao katika kipindi cha miaka 50
ya Uhuru ni wanawake miaka 50 ya uhuru, tumethubutu, tumeweza
na sasa tunasonga mbele.
|