Wanawake
watakiwa kutumia nafasi wanazopewa na UNIFEM, October 30, 2011
Na Anna Nkinda- Perth Australia
Wanawake wametakiwa kutumia nafasi zinazotolewa na Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wanawake (UNIFEM) katika
kujiletea maendeleo yao na ya mataifa yao kwani lengo kuu la kuanzishwa
kwa shirika hilo ni kumuinua mwanamke na kuleta usawa wa kijinsia.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Dk.
Noeleen Heyzer wakati akiongea na wake wa wakuu wa nchi wanachama
wa Jumuia ya Madola katika mkutano wao uliofanyika Perth nchini
Australia.
Dk. Heyzer alisema kuwa hivi sasa katika nchi nyingi Duniani
wanawake wanapewa nafasi za kupata elimu, kuwezeshwa kiuchumi,
usawa wa kijinsia , kupata afya bora kwa mama na mtoto na upatikanaji
wa ajira hii yote ni kumfanya mwanamke aweze kujiinua kiuchumi
kwani hapo zamani wanawake walikuwa wameachwa nyuma kimaendeleo
tofauti na wanaume.
“UNIFEM inashughulika na masuala ya usawa wa jinsia na uwezeshaji
wa wanawake kiuchumi, kisiasa na kijamii hivyo basi ni jukumu
lenu kuwahamasisha wanawake katika nchi mnazotoka ili waweze kuzitumia
nafasi wanazopewa hii itawasaidia kujikwamua kiuchumi”, alisema
Baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa UNIFEM kumaliza kuongea na wake
hao wa wakuu wan chi akiwemo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete walitembelea
Halmashauri ya jiji la Perth upande wa Sekta ya Nishati na Madini
na kuelezwa jinsi sekta hiyo ilivyochangia kutoa ajira na kuinua
uchumi wa nchi hiyo.
Viongozi kutoka makampuni ya uchimbaji wa madini ambao ni Mtendaji
Mkuu wa Chamber of Minerals and Energy of West Australia Reg Howard-Smith,
Mkurugenzi Mtendaji wa Argyle Diamonds Kevin McLeish na Josephine
Archer ambaye ni meneja biashara kutoka Argyle Pink Diamonds walisema
kuwa kutokana na jiografia nzuri mji huo umejaliwa kuwa na madini
mengi ukilinganisha na miji mingine.
“Upande wa Magharibi wa Nchi yetu kuna miji minne ambayo ni Kimberley,
Pilbara, Yilgarn na Kusini Magharibi ambako kunapatikana madini
zaidi ya aina 50 baadhi yakiwa ni dhahabu, almasi, chuma, mchanga
mzito wenye madini aina tofauti, base metals, chumvi, chuma cha
pua, Ilmenite, Rutile, Alumina, Zircon, Garnet na Tantaluma”,
walisema.
Wake wa wakuu wan chi wanachama wa Jumuia ya madola waliweza
kujionea aina mbalimbali za madini yanayopatikana katika nchi
hiyo pamoja na vito vya thamani na bidhaa zinazotengenezwa kutokana
na madini hayo.
Aidha waliweza kutembelea bustani ya kutunza mimea na wanyama
wa asili nakuona jinsi viumbe hai vya kale vinavyotunzwa ili visiweze
kupotea kwa ajili ya kumbukumbu ya vizazi vijavyo na wageni wanaotembelea
nchi hiyo.
Mkutano wa wakuu wa Nchi wanachama ya Jumuia ya madola umemalizika
leo na Kaulimbiu ya mwaka 2011 ya Jumuia hiyo ni “Wanawake ni
wakala wa mabadiliko”.
|