Mama
Kikwete awataka wanafunzi kutokuchanganya elimu na mapenzi, September
26,2011
Na Anna Nkinda – Maelezo
Wanafunzi nchini wametakiwa kuachana na tabia ya kujiingiza katika
mapenzi wakiwa masomoni kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanahatarisha
maisha yao kwa kupata maambukizi ya Virusi vinavyosababisha Ugonjwa
wa Ukimwi na ujauzito.
Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Kikwete wakati akiongea
na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana ya Barbro Johansson
iliyopo Luguruni jijini Dar es Salaam kwenye sherehe za mahafali
ya kidato cha nne na cha sita.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake
na Maendeleo (WAMA) aliwaambia wanafunzi hao kuwa elimu wanayoipata
itafungua maisha yao na ya jamii nzima. Itawapa njia ya kuwa na
uwezo kiuchumi, itawajengea uwezo wa kujiamini na kuweza kupaza
sauti zao na kusikika kwani watakuwa na upeo mkubwa wa kuchambua
mambo na kutoa maamuzi ya busara katika maisha.
“Ninafahamu kwamba walimu, wazazi na walezi wamekuwa wakiwausia
na kuwapa miongozo katika maisha yenu ya kutafuta elimu. Jambo
ambalo ningependa muendelee kulizingatia kwa makini ni kwamba
elimu mliyoipata bado ni mwanzo tu, hasa ukizingatia kukua kwa
utandawazi.
Siku hizi mabadiliko ni ya haraka mno na yanamgusa kila mtu katika
kila nyanja ya maisha. Ni vizuri mkajua kwamba ni wajibu wenu
kuendelea kujifunza mbinu mpya za kuyakabili mabadiliko haya”,
alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alimalizia kwa kuwataka wanafunzi hao
kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi kwani elimu waliyonayo
haitakuwa na maana kama wataruhusu kuambukizwa ugonjwa huo na
kupata ujauzito ambao utawafanya wakatize masomo yao na hivyo
kutotimiza ndoto zao.
Akisoma taarifa ya shule hiyo Mkuu wa Shule Halima Kamote alisema
kuwa tangu kuanzishwa kwa shule hiyo miaka 11 iliyopita jumla
ya wahitimu 471 wa kidato cha nne na 282 wa kidato cha sita walihitimu
masomo yao na kufaulu kwa kiwango cha juu na kufanikiwa kujiunga
na vyuo mbalimbali na vya elimu ya juu hapa nchini.
Kamote alisema , “Katika mahafali ya leo tunao wahitimu 76 wa
kidato cha nne na 151 wa kidato cha sita ambao tunaamini kutokana
na elimu waliyoipata kutoka kwa walimu wao watafanya vizuri katika
mitihani yao ya kitaifa na hivyo kuendelea kutunza heshima ya
shule yetu katika jamii”.
Shule hiyo yenye wanafunzi 632 wa kidato cha kwanza hadi cha
sita, walimu 37 na wafanyakazi wengine 27 imekuwa ikipata msaada
kutoka Serikali ya Sweden kupitia ubalozi wake hapa nchini ambao
umetumika kujenga majengo, matanki ya kuhifadhi maji na kutoa
ufadhili kwa wanafunzi wenye vipaji kilaaluma ambao wanatoka katika
familia zenye kipato duni.
Alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni upungufu wa
majengo, wafadhili wakuu wa shule hiyo ambao ni SIDA wanatarajia
kukatisha ufadhili wao mwishoni mwa mwaka huu na hivyo kuzua tatizo
la kukosekana kwa ufadhili wa uhakika wa ada kwa wanafunzi wanaotoka
katika familia duni.
“Changamoto nyingine zinazotukabili ni wanafunzi wanaofadhiliwa
na shule hii wanakosa mikopo pale wanapojiunga na elimu ya juu
pengine ni kwa kuwa wanatoka katika shule binafsi ambako kuna
ulipaji wa ada unaoendana na gharama halisi na mahitaji ya kujiunga
na shule ni makubwa kuliko uwezo wa shule”, alisema.
Kila mwaka sherehe za mahafali ya shule hiyo hufanyika tarehe
25 Septemba ili kuienzi siku aliyozaliwa Dk. Mama Barbro Johansson
ambaye ni mmisionari, mwalimu, mwanaharakati na mwanadiplomasia
kutoka nchini Sweden ambaye alitoa mchango mkubwa katika kupigania
elimu ya watoto wa kike na wa kiume.
|