Wanafunzi 287 wapata ujauzito Kwa kipindi cha miezi Tisa mkoani Pwani
Na Anna Nkinda – Maelezo, Kibaha- 04/10/2009 Jumla ya wanafunzi 287 wamepata ujauzito kwa kipindi cha miezi tisa katika mkoa wa Pwani na hivyo kushindwa kumaliza elimu ya msingi na sekondari.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa huo Hajati Amina Mrisho Said wakati akisoma taarifa ya maendeleo ya mkoa kwa mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliyetembelea shule ya Sekondari Magindu iliyopo wilayani Kibaha kwa ajili ya kutoa msaada wa magodoro 100 na vitanda vyake.
Hajati Amina alisema kuwa wilaya ya Rufiji inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliopata ujauzito kwani kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu wanafunzi 130 wamepata ujauzito ambapo wanafunzi wa Shule ya Msingi ni 110 na Sekondari ni 20.
Aliitaja wilaya ya Mafya kuwa haina tatizo kubwa la wanafunzi kupata ujauzito ukilinganisha na wilaya zingine kwani kwa mwaka huu waafunzi wa shule ya Msingi watatu na sekondari kumi ndio waliopata uajauzito.
Tatizo lingine linaloukabili mkoa huo kuhusiana na mambo ya elimu ni utoro mashuleni, upungufu wa miundombinu, upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika shule za sekondari na upungufu wa vitanda na magodoro katika sekondari zenye hosteli.
" Ili kukabiliana na matatizo hayo mkoa wetu umeanza kujenga Hosteli katika shule zote za sekondari za kutwa kwani tuna shule za kutwa za serikali 94 kati ya hizi zenye hosteli ni 31 tu", alisema.
Hatua zingine wanazozichukua ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, ushirikiano wa wazazi na walimu, ufuatiliaji katika ngazi zote za mitaa, vijiji, kata na wilaya, Hamashauri zimeanzishwa sheria ndogo na zinafuatwa kikamilifu, kuchukua hatua kwa watu wanaowapa mimba wanafunzi na kuhamasisha utoaji wa chakula cha mchana.
Naye Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa elimu ni jambo la muhimu sana katika maendeleo ya mwanadamu na jamii yake kwani hakuna jamii ambayo imepiga hatua ya maendeleo bila ya kuwa na elimu.

"Ninawaomba wazazi na wanajumuia ya Magindu kuwaendeleza watoto wenu kielimu hasa watoto wa kike ambao siku za nyuma hawakuwa wanathaminiwa vilivyo kwani huu ndio urithi endelevu usioweza kuibiwa wala kuharibika", alisema.
Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwataka wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii na kutokujiingiza na mambo ya mapenzi wangali shuleni kwani wanaume watadanganywa na kuwachezea na wakishapata ujauzito watakatisha masomo yao na kutokutimiza ndoto zao.
Mama Kikwete alisema, "Nanyi wazazi msikubali kulimaliza tatizo la mimba kienyeji pale ambapo mtoto wako atakuwa amepata ujauzito ninachowashauri ni kufuata taratibu na kisheria kwa kutoa taarifa Polisi jambo litakalosababisha mwanaume aliyempa ujauzito binti yako aweze kuchukuliwa hatua kali".
Kutokana na tatizo la utoro wa wanafunzi aliwashauri wazazi wa watoto wanaosoma shuleni hapo kuchangia chakula shuleni hasa wakati wa mavuno jambo ambalo litawafanya wanafunzi kupata chakula shuleni na hivyo kupunguza tatizo la utoro hivi ndivyo wanavyofanya katika maeneo mengi hapa nchini.
Akisoma taarifa ya shule ya Sekondari Magindu Mwalimu Mkuu Shiloto alisema kuwa shule hiyo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne 468 kati ya hao wanawake ni 198 na wanaume ni 270 na idadi ya walimu ni 12.
Mwalimu huyo aliyataja mambo yanachangia kufeli wanafunzi katika mitihani yao ni upungufu wa walimu, utoro wa wanafunzi, upungufu wa zana za kufundishia, kutokupatikana kwa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa na uelewa mdogo wa wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa elimu.
Mwalimu Shiloto alisema, "Changamoto inayozikabili shule hii ni walimu wa masomo ya sayansi, , nyumba za walimu, tupungufu wa vyumba vya madarasa, shule haina bwalo, maabara, maktaba, maji , umeme na usafisi wa uhakika".
Alilitaja tatizo la wasichana kupata ujauzito na hivyo kushindwa kuendelea na masomo kwani tangu mwaka 2007 mpaka sasa jumla ya wanafunzi 21 wa vidato mbalimbali waliacha shule kwa sababu ya tatizo hilo .
Mama Kikwete anafanya ziara ya kikazi ya siku sita katika mkoa wa Pwani kwa lengo la lengo la kuchangia juhudi za kupunguza vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi kwa kutoa vifaa vya huduma ya afya ya uzazi, hususan katika wodi za wazazi. Kuhamasisha juhudi za maendeleo kwa wanawake kupitia vikundi vya SACCOS na benki za vijijini- VICOBA.
|